Mwimbaji nyota wa muziki wa bongo fleva Isihaka Nassoro, ‘Aslay’ rasmi ametangazwa kujiunga na Sony Music Entertainment Africa baada ya mda mrefu kupita bila ya msanii huyo kusikika akitamba kama ilivyokuwa hapo awali.
Aslay , ameingia kwenye headline kufuatia kupotea kwake kwenye muziki kwa kipindi kirefu bila ya kubainishwa hadharani sababu zilizopelekea nyota huyo kukaa kimya, jambo lilisababisha kuibuka kwa uvumi wa namna mbali mbali kutoka kwa mashabiki.
Baada ya Aslay kujiunga rasmi na Sony Music, Mkuu wa Sony Music ukanda wa Afrika Mashariki, Christine “Seven” Mosha, aliweka bayana hisia zake juu ya nyota huyo na kile ambacho wamekipanga katika kuhakikisha talanta yake inaendelea kukua na kufika mbali zaidi.
“Ninajivunia kuwa na msanii wa hadhi ya Aslay kuungana nasi Sony Music Africa, Aslay ni mwimbaji na mtunzi wa kipekee ambaye ameongoza aina ya muziki wa Bongo flava kote barani Afrika na sasa ulimwenguni kote, tunafurahi kushirikiana naye kuleta talanta yake ya ajabu na muziki masikioni mwa mashabiki wengi tuwezavyo ulimwenguni.” amesema Seven.
Aslay anatajwa kama mmoja wa wasanii wenye umri mdogo aliyefanikiwa kujizolea idadi kubwa ya mashabiki wa kila umri barani Afrika kutokana na umahiri wake katika muziki na mpaka sasa nyota huyo ana jumla ya wafuasi milioni 5 kwenye ukuras wake wa instagram, Milioni mbili kwenye ukurasa wake wa Facebook, pamoja na wafuasi wasiopungua Milioni moja kwenye chaneli yake ya YouTube.
‘Napenda kuwaambia mashabiki wangu kuna kazi mpya zinakuja kwa hiyo kaeni tayari kwa album, kaeni tayari kwa nyimbo, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu, nachoweza kusema ni kuwaambia tu watu ambao wanapenda kuona Aslay anafika mbali wategemee kazi nzuri kutoka kwangu nishaingia mzigoni kwa hiyo hakuna mambo mabaya, sasa hivi tutegemee vitu vizuri” amesema aslay.