Kiungo mkabaji wa Azam FC, Sospeter Bajana, amesema hatasahau rekodi ya kufunga mabao mawili katika mechi moja ambayo iliiweka Novemba 4 mwaka huu wakati timu yake ilipopata ushindi wa magoli 3-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya wenyeji Ihefu FC.
Bajana amesema hajawahi kufunga mabao mawili katika mechi moja tangu aanze kucheza soka, hivyo kwake ni jambo la kukumbukwa daima.
Kiungo huyo amesema rekodi hiyo atatembea nayo katika maisha yake ya soka, hasa ikizingatiwa yeye anacheza eneo la kiungo mkabaji, hivyo amekuwa hafungi sana mabao na hata ikitokea anafunga goli moja tu.
“Yaani nashukuru Mungu, unajua hii ni mara yangu ya kwanza katika maisha yangu, nilikuwa sijawahi kufunga mabao mawili kwenye mechi moja tangu nianze kucheza soka, siku ya Novemba 4, mwaka huu nitaiweka katika kumbukumbu yangu ya soka hadi nastaafu, ni rekodi bora sana kwangu hasa ikizingatiwa kiungo wakabaji jukumu lao la kwanza si kufunga mabao,” amesema Bajana
Kuhusu mwenendo wa timu yake, amesema kwa sasa imerejea katika ‘reli’ baada ya kushinda mechi mbili mfululizo tena ikiwa ugenini.
“Kusema kweli tumerudi katika morali, tulipoteza mechi mbili mfululizo, tukakaa wenyewe kama wachezaji na kujiambia tuvute soksi tupambane, ndiyo tukaanza sasa kupata ushindi katika mechi mbili mfululizo,” amesema mchezaji huyo.