Gwiji wa Soka nchini England Rio Ferdinand amemponda Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya nchi hiyo ‘The Three Lions’ Gareth Southgate baada ya kutomjumuisha winga wa Chelsea, Raheem Sterling kwenye kikosi chake.
Beki huyo wa zamani wa Manchester United alikasirishwa baada ya kocha kumpotezea Sterling kwa ajili ya mechi zijazo za kufuzu Euro 2024.
Rio alimkashifu Southgate akieleza kuwa nyota huyo wa Chelsea ametoa mchango mkubwa wa mabao msimu huu kuliko Jack Grealish na Marcus Rashford kwa pamoja.
Nyota huyo wa zamani wa Manchester City na Liverpool hajaichezea England tangu mechi ya robo fainali ya Kombe la Dunia dhidi ya Ufaransa Desemba mwaka jana.
Mchezaji huyo aliumia katika mechi za kwanza za kufuzu za Euro 2024 Machi mwaka huu, na baadae Southgate akampotezea mara nne mfululizo.
Akiongea kwenye chaneli yake ya YouTube ya Five, beki huyo wa zamani wa England alisema: “Wamuachie huru Sterling. Mwachilie kijana wangu, Raheem Sterling. Sijui amefanya nini, sijui ni kitu gani kimetokea.
“Kukosekana kwake kwenye kikosi cha England inashangaza sana. Ndio kuna vipaji vingi sana, msinielewe vibaya. Lakini kama tunazungumzia kiwango, Sterling ana mabao mengi na asisti, na mchango mkubwa kuliko Rashford na Grealish kwa pamoja.”
Vijana wa Southgate, ambao tayari wamekata tiketi ya kushiriki michuano ya Ulaya (Euro) mwakani, watamenyana dhidi ya Malta kesho Ijumaa (Novemba 17) kabla ya kukabiliana na Macedonia ya Kaskazini siku tatu baadae.
Sterling amekuwa hatari kwenye kikosi cha Mauricio Pochettino kutokana na mchango wake Chelsea ilipata matokeo chanya mechi za hivi karibuni ikiwamo sare ya mabao 4-4 dhidi ya Man City mwishoni mwa juma lililopita ambayo aliwasumbua sana mabingwa hao wa Ligi Kuu ya England.