Spika wa Bunge la Somalia amejiuzulu baada ya wiki mbili za harakati za baadhi ya wabunge kutaka kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye.
Wabunge wameeleza kuwa Spika amechukua hatua hiyo jana wakati ambapo wabunge zaidi ya 100 walisaini mpango wa kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye mwezi Machi.
“Naibu Spika alitusomea taarifa na tamko kuwa Spika Mohamed Sheik Osman Jawari amejiuzulu. Hatua hii imewatuliza wabunge na kuondoa kabisa mgogoro uliokuwepo,” mbunge Dahir Jesow aliliambia shirika la habari la AFP.
Jesow amesema wengi wanamshukuru kwa hatua aliyoichukua spika hiyo. Amesema Bunge linapaswa kufanya uchaguzi wa spika mpya ndani ya taratibu za kikatiba mapema iwezekanavyo.
Mpango uliosainiwa na wabunge mwezi Machi ulizua mgogoro pia kati ya wabunge 275 wa bunge hilo. Baadhi ya wabunge waliokuwa wamesaini waliomba kuondoa tena sahihi zao dakika ya mwisho, hali iliyozua sintofahamu.
- Kesi ya kuondolewa ukomo wa umri wa urais Uganda ‘yawaka’
- Marekani kuchukua maamuzi magumu dhidi ya Syria
Serikali ilimtaka mara kadhaa Spika huyo kujiuzulu lakini alikataa kwa madai kuwa taratibu za kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye unapaswa kufuatwa. Alituhumu Serikali kwa kuweka askari polisi wengi katika majengo ya bunge kwa lengo la kumtishia.
Taharuki iliongezeka mitaani na barabara muhimu zilifungwa wakati vuguvugu la mvutano kati ya Serikali na wabunge wanaoiunga mkono wakisuguana na wale wanaomuunga mkono Spika huyo.