Spika wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Dkt. Martin Ngoga ameishukuru na kuipongeza Serikari ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ukiwemo wa reli kwa sababu inaleta manufaa hata kwa nchi jirani.
“Miradi hiyo ambayo kwa sasa inatekelezwa kwa kasi si kwamba inachochea ukuaji wa uchumi wa Tanzania, bali hata wa nchi nyingi za jirani kwa kuwa nazo zitanufaika na miradi hiyo kwani si nchi zote zina bandari”.
Dkt. Ngoga ameyasema hayo leo 23, 2018 alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Bungeni mjini Dodoma.
Amesema tayari wamejadili ripoti iliyotokana na ziara iliyofanywa na wabunge hao katika upande wa korido ya kusini na korido ya kaskazini ambapo wametoa mapendekezo yatakayofanyiwa kazi na baraza la mawaziri.
“Tayari tumeshajadili miswada miwili inayohusu Itifaki ya Sarafu Moja ambayo ni mswada wa taasisi ya Fedha na mswada wa Takwimu yote ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2017.”
Pia Spika huyo amesema wamefurahia uwepo wao nchini, ambapo mbali na shughuli zao za kibunge pia kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma wameshiriki kampeni ya kuifanya Dodoma kuwa ya kijani kwa kupanda miti 1,000 kwenye eneo la Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Kwa upande wake, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema amefarijika na uamuzi wa Bunge la EALA kufanya vikao vyake katika nchi wanachama kwa sababu unatoa fursa ya kujua mazingira ya nchi hizo pamoja na maendeleo yake.
Amesema nchi wanachama wanamatumaini makubwa na bunge hilo katika kuimarisha na kuboresha maendeleo ya mataifa yao, hivyo amewatakia mjadala mwema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewakaribisha wabunge hao na marafiki zao kuja kuwekeza kwenye sekta mbalimbali nchini ikiwemo ya viwanja, utalii, kilimo na madini.
Kwa mara ya kwanza vikao vya Bunge la Afrika Mashariki, (EALA) vinafanyika Dodoma katika ukumbi wa Bunge wa Msekwa uliopo ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Vikao hivyo vilianza Aprili 17, 2018 na vinatarajiwa kumalizika Aprili 29, 2018.