Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amesema kuwa kitendo cha aliyekuwa mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea kutangaza kujiuzulu ndani ya Bunge sio kinyume cha sheria na kanuni.
Akijenga hoja kuhusu ufafanuzi huo, Spika Ndugai alikumbusha kitendo hicho na uamuzi uliowahi kuchukuliwa mwaka 2008 na aliyekuwa Waziri Mkuu wa wakati huo, Edward Lowassa ambaye alisimama ndani ya Bunge na kutangaza kujiuzulu.
“Mtolea hakufanya kosa, hakuna kosa lolote kisheria. Hata Lowassa alitangaza kujiuzulu ndani ya Bunge,” Ndugai aliiambia Radio One.
Alifafanua kuwa kitendo hicho kingekuwa na mashaka au makosa endapo Mtolea angekuwa amelazimishwa kufanya hivyo, lakini alitangaza hatua hiyo kwa hiari yake.
-
Hatua kali kuchukuliwa dhidi ya watakaoingiza bidhaa za magendo nchini
-
Spika Ndugai ampiga kijembe Msigwa ‘Najua roho inamuuma sana’
Jana, Mtolea alitangaza kujiuzulu nafasi yake kwa sababu alizoeleza kuwa ni mgogoro mkubwa unaofukuta ndani ya Chama Cha Wananchi (CUF), na kwamba ulikuwa kikwazo katika kutekeleza ipasavyo majukumu yake kama Mbunge.
Aidha, alivialika vyama vya siasa ambavyo viko tayari kufanya naye kazi kuzungumza naye. Wito huo ulihitimishwa jana usiku baada ya mwanasiasa huyo kutangaza rasmi kujiunga na Chama Cha Mapinduzi, mbele ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Dkt. Bashiru Ally.