Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai ameridhia kufutwa uanachama kwa Wabunge nane wa Viti Maalum kutoka Chama cha Wananchi (CUF) na kutangaza nafasi zao kuwa wazi.
Hayo yamejiri baada ya hivi karibuni Spika huyo kupokea barua kutoka kwa Mwenyekiti wa CUF Taifa anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili, Profesa Ibrahim Lipumba inayoeleza kuwafukuza uanachama Wabunge hao na Madiwani wawili kwa makosa mbalimbali yakiwemo ya kinidhamu, kukihujumu chama, Kumkashifu na kumdhalilisha Mwenyekiti.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya Bunge imeeleza kuwa Spika Ndugai amejiridhisha kuwa Wabunge hao wamefutiwa uanachama kulingana na taratibu za chama hicho na hivyo hawana sifa za kuendelea na Ubunge.
Hivyo, kwa mamlaka aliyonayo kwa kuzingatia kifungu cha 67(1)(b) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 kikisomwa pamoja na kifungu 37(3) cha Sheria ya Uchaguzi Sura ya 343 kama ilivyojadidiwa Mwaka 2015, Spika ametangaza nafasi hizo kuwa wazi na kumuandikia Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi aendelee na hatua zinazostahili kujaza nafasi hizo kwa mujibu wa Sheria.