Kampuni ya mchezo wa bahati nasibu SportsPesa imesema kuwa itasitisha udhamini wote iliyowekeza katika ligi kuu ya nchi hiyo KPL mara baada ya Serikali ya Kenya kuongeza kodi inayolipwa.
Hayo yamesemwa na Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo nchini humo, Ronald Karauri mara baada ya kupewa taarifa ya ongezeko la kodi ya asilimia 35% ambayo watatakiwa kulipa katika kila msimu wa ligi kuu nchini humo KPL.
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa shirikisho la mpira nchini Kenya, Jack Oguda amesema kuwa kama SportsPesa watachukua hatua hiyo, basi kutakuwa na athari kubwa katika ligi hiyo.
Aidha, kodi hiyo imeidhinishwa na Serikali ya Kenya ili kuweza kuwadhibiti watoto na vijana wadogo kujihusisha na kushiriki katika mchezo huo wa kubashiri ambao umekuwa ni gumzo nchini humo.
Hata hivyo, Wakenya wengi wameonekana kuwa ni miongoni mwa watu wanaoshiriki sana katika mashindano ya mchezo wa kubahatisha katika nchi zilizopo kusini mwa jangwa la Sahara.