Idadi ya vifo vitokanavyo na mlipuko wa mabomu kwenye makanisa na hoteli za kifahari nchini Sri Lanka Jumapili ya Pasaka, imeongezeka hadi kufikia 290 kwa mujibu wa vyombo vya usalama.
Polisi wa nchi hiyo wameeleza kuwa watu 24 wanashikiliwa na kuhojiwa kutokana na tukiio hilo lakini Serikali bado haijataja kundi au watu wanaohusika na mashambulizi hayo.
Zaidi ya watu 500 wameripotiwa kujeruhiwa ikiwa ni pamoja na makumi ya raia wa kigeni, katika shambulizi hilo ambalo linatajwa kuwa baya zaidi kuwahi kutokea nchini humo tangu kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2009.
Ripoti zinaeleza kuwa mitandao ya kijamii imezimwa kwa muda nchini humo na mawasiliano ya WhatsApp hayapatikani kwa wengi ili kuzuia kusambaa kwa taarifa zinazokanganya, kuingilia upelelezi na kuongeza taharuki.
Ripoti ya kwanza ilieleza kuwa mlipuko ulianza majira ya saa mbili asubuhi kwa saa za nchi hiyo, ambapo mabomu sita yalipotiwa katika eneo moja dogo.
Makanisa matatu makubwa yalishambuliwa katika maeneo ya Negombo, Battlicaloa na Colombo wakati waumini wakiendelea na ibada ya Pasaka. Milipuko mingine ilishambulia hoteli za kifahari za Shangri-La, Kingsbury na Cinnamo zilizopo katika mji mkuu wa nchi hiyo.
Wakati polisi wakianza kuwasaka wahusika, milipuko mingine miwili iliripotiwa kwa nyakati tofauti. Mlipuko mmoja uliripotiwa karibu na hifadhi ya wanyama ya Dehiwala, Kusini mwa Colombo. Bomu la nane liliripotiwa karibu na wilaya ya Dematagoda baada ya polisi kuvamia eneo hilo, maafisa watatu walipoteza maisha.