Klabu ya soka ya SSC Napoli ya Italia, imekataa kuomba radhi kwa kutoa video ya utani kwa kumlenga Victor Osimnhen, lakini ilisisitiza kwamba hawakuwa na mpango wa kumkosea adabu mshambuliaji wao.
Miamba hiyo ya ‘Serie A’ ilipandisha video kwenye mtandao wake wa Tik Tok ikonyesha kumkebehi Osimhen, kitu ambacho kilisababisha wakala wake kutishia kuchukua hatua za kisheria.
Video hiyo ilikuwa ikimwonyesha nyota huyo mwenye miaka 24, akiomba Penati, huku kukiwa na sauti ya ajabu kama inayotoka kwa Osimhen ikisema Naomba Penati tafadhali kabla ya mkwaju wake kutoka nje ya lango.
Video ya pili kwenye akaunti ya klabu hiyo, ambayo ilikuwa ikisambaa mitandaoni kabla ya kufutwa, ikimfananisha Osimhen ‘nazi’.
Hilo lilimfanya wakala wa Osimhen kudhani kuwa kuna haja ya kuchukua sheria.
Katika taarifa yake ya SSC Napoli ilikuja na kauli yake na kusema: “SSC Napoli, inapenda kuepuka masuala yote ya utata, ikimaanisha kuwa haikuwa na nia ya kumkebehi Victor Osimhen, ambaye ni hazina ya klabu.”
Klabu hiyo pia ilijaribu kufafanua jinsi ilivyokataa ofa mbalimbali nono zilizoletwa kwa ajili ya kumuuza mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Nigeria mwezi uliopita.
“Kwa kuthibitisha hilo, wakati wa dirisha la usajili lililopita, klabu ilikataa ofa nyingi na nono zilizoletwa mezani kwa ajili yake. Hiyo ni kwa sababu ni mchezaji muhimu hapa,” ilisema sehemu ya taarifa ya SSC Napoli.