Mamlaka ya Udhibiti wa Mifuko ya Jamii (SSRA), imepanga kuwafikia wanachama wake wote nchini kuwaelimisha kuhusu kikokotoo kinachotoa 25% za mkupuo wa mafao kwa wastaafu.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dkt. Irene Isaka jana aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa kutopata elimu ya kutosha kuhusu hatua hiyo ya Serikali kumewafanya wastaafu kutoelewa nia yake ya kuwaneemesha kupitia kanuni mpya.
“SSRA tumejipanga kuwafikia wanachama wote nchini na kuwapa elimu juu ya kanuni hii mpya ya ukokotoaji wa mafao ili kuwaondoa katika hofu ambayo imejengeka miongoni mwao kutokana na maneno ya baadhi ya watu wasio na uelewa wa kutosha juu ya kanuni mpya ya ukokotoaji mafao,” alisema Dkt. Isaka.
Alieleza kuwa kutokana na mabadiliko hayo, watawawezesha wastaafu kuendelea kupata mishahara yao katika kipindi chao chote cha maisha, tofauti na awali ambapo walikuwa wakichukua fedha nyingi kwa mkupuo na baadaye kujikuta wanaishi maisha magumu.
Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) pamoja na baadhi ya wadau walipinga vikali kanuni mpya za mafao hususan utoaji wa 25% kwa wastaafu.