Shirika la Madini la Taifa – STAMICO, limenyakua tuzo ya Kampuni bora ya mwaka Afrika kwenye sekta ya madini 2023 katika tuzo za Africa Company of the Year Award – ACOYA.
Akipokea tuzo hiyo kwa niaba ya Shirika, Mkurugezi Mtendaji Dkt. Venance Mwasse ambaye aliambatana na Menejimenti ya STAMICO, alisema tuzo hiyo imedhihirisha juhudi za shirika hilo katika kuinua sekta ya madini nchini.
Amesema hatua ya STAMICO kuwa kampuni bora kwa mwaka 2023 imekuwa chachu kwa shirika hilo kuongeza kasi ya utendaji ili kuwanufaisha Watanzania na kuongeza kuwa, “zaidi ya nchi 15 kutoka bara la Afrika zilishiriki kwenye kuwania tuzo hizi na STAMICO iliweza kuibuka kidedea kama Kampuni Bora ya Madini Afrika.”
STAMICO imekuwa mfano wa kuigwa Afrika kiasi cha kuivutia Wizara ya Madini na Uchumi wa Buluu ya Kenya, huku Viongozi Waandamizi wa Wizara hiyo wakija nchini kujifunza namna STAMICO inavyoendeleza shughuli za uchimbaji madini na namna ilivyofanikiwa kuendesha shughuli za madini ikiwemo utafiti, uchimbaji, uchakataji, na biashara ya madini
Akizungumza katika hafla ya utoaji tuzo hizo, Mkurugenzi wa Africa Company of The Year Awards (ACOYA), Deogratius Kilawe tuzo hizo zinajulikana kama Africa Company of the year Awards (ACOYA), mwaka huu 2023 ndio mara ya kwanza tuzo hizo kutolewa hapa Tanzania.
Aidha, Kilawe alizipongeza na kuzishukuru kampuni zote zilizoshiriki na kushinda na kusema lengo la tuzo hizo ni kuongeza ufanisi kwa kampuni katika utoaji huduma kwa wateja wao na wafanyakazi ili kuongeza uwajibikaji kazini huku akisema, “mwisho wa tuzo hizi ni mwanzo wa maandalizi wa tuzo zijazo tunachukua changamoto zilizojitokeza mwaka huu kuboresha tuzo zijazo.”
Tuzo hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wageni mbalimbali huku mchakato wa kutafuta washindi ukiwa umefanywa na Kampuni ya Eastern Star Consulting Group Afrika ya nchini Kenya.