Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limesainiana mkataba wenye thamani ya shillingi Bilioni 4 wa kandarasi ya uchorogaji miamba na Kampuni ya Madini ya Buckreef Gold Company Ltd inayochimba madini ya Dhahabu mkoani Geita.
Makubaliano hayo yamefanyika katika ofisi za STAMICO, jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Wizara ya Madini na STAMICO huku Mgeni rasmi katika tukio hilo ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof Simon Msanjila.
Katika hotuba yake Katibu Mkuu amelipongeza Shirika la Madini la Taifa kwa kazi nzuri wanayofanya ya uchorogaji ambayo imewafanya kupata tena kandarasi kubwa ya uchorogaji.
“Kandarasi hii ni kubwa kwa hiyo fanyeni kazi hii kwa viwango vya juu kwa kutumia ujuzi wenu wote, uaminifu na bidii,” Amesema Katibu Mkuu.
Naye Kaimu Mkurugezi Mtendaji wa STAMICO, Dr Venance Mwasse ameishukuru Wizara ya Madini kwa kuendelea kuiamini STAMICO na kumhakikishia, Katibu Mkuu kufanya kazi hiyo ya uchorogaji kwa weledi na kwa kufuata vigezo vyote vilivyopo kwenye mkataba.
Naye Mkurugenzi wa kampuni ya Buckreef, Khalaf Rashid ameishukuru Wizara ya Madini na STAMICO kwa kuendelea kufanya kazi kwa karibu na kampuni ya Buckreef.