Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Shirika la Umeme Tanzania TANESCO wametia Saini Hati ya Makubaliano ya miaka miwili kutekeleza mradi wa kuzalisha umeme wa megawati 200 kwa kutumia makaa ya mawe yanayopatikana Kiwira mkoani Songwe ikiwa ni hatua ya awali utekelezaji wa mradi huo.
Katika utekelezaji wa mradi huo STAMICO itahusika na ujenzi wa mgodi wa wazi wa kuchimba makaa ya mawe, wakati TANESCO itahusika na ujenzi wa mtambo wa kuzalisha umeme wa MW200 (Power Plant) sambamba na njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kV 400 kutoka Kiwira kwenda Mwakibete na kuunganisha na gridi ya Taifa.
Aidha makubaliano yamefikiwa na mashirika hayo baada ya kukamilika kwa zoezi la utiaji saini wa Hati ya Makubaliano uliofanyika ofisi za TANESCO Makao Makuu Jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi na wataalamu kutoka katika Taasisi hizo mbili.
Akielezea umuhimu wa makubaliano hayo Kaimu Mkurugenzi wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse, amesema utekelezaji wa mradi huo unaenda kuyaongezea thamani madini ya makaa ya mawe kwa kuwa kwa muda mrefu yamekuwa hayatumiki kimamilifu katika uzalishaji wa umeme kwa ajili ya kulisha kwenye gridi ya Taifa.
Aidha Kaimu Mkurugenzi Mwasse ameushukuru uongozi wa uongozi wa TANESCO kwa kushirikiana bega kwa bega tangu STAMICO ilipoanza mchakato wa kuhuisha mradi unaolenga kuokoa rasilimali madini zilizopo katika mgodi ili ziweze kuwanufaisha watanzania.
Naye Mkurugenzi Mtendaji TANESCO Mhandisi Tito Mwinuka, amesema makubaliano hayo ni hatua ya awali inayotoa nafasi kwa kila Taasisi kufanya majukumu yake, ambapo hatua inayofuata ni kufanyika kwa upembuzi yakinifu ili kuweza kubainisha mambo mbalimbali ikiwemo teknolojia na gharama halisi ya utekelezaji wa mradi huu.