Siku moja baada ya kampuni ya Acacia Gold Mine ya Bulyanhulu mkoani Shinyanga kuthibitisha taarifa za kuvunja mkataba na Stand Utd FC, uongozi wa klabu hiyo umedai haufahamu chohote, kwani mpaka sasa haujapata barua rasmi kutoka kwa wadhamini hao.

Jana afisa mawasiliano wa Acacia Gold Mine, Hectar  Pendaeli Poya alisikika kwenye vyombo mbalimbali vya habari nchini akitangaza kuvunja mkataba na klabu hiyo kwa kuwa imekuwa na migogoro isiyokwisha.

Stand United inakiri kusikia taarifa za uvunjwaji wa mkataba wao huo kupitia vyombo mbalimbali vya habari nchini, lakini bado hawajapokea kwa maandishi taarifa hizo.

Afisa Habari wa timu hiyo, Deokaji Makomba amesema kwamba  hawajapokea taarifa yoyote rasmi kutoka kwa wadhamini wao hao aliowaita wapendwa.

“Sisi kama Accacia Stand United Chama la Wana hatujapokea taarifa yoyote officially (rasmi) kwamba wadhamini wetu wapendwa, kampuni ya uchimbaji madini ya dhahabu Accacia ambao wanachimba madini katika mgodi wa Shinyanga, wamejitoa kuweza kuidhamini timu yetu bado hatuja pokea taarifa hii rasmi” alisema Makomba.

Hata hivyo msemaji huyo alielezea na kukiri kuzisikia taarifa zilizotolewa na Accacia.

“Taarifa ambazo tumekuwa tukizisikia kwenye baadhi ya vyombo vya habari na ni kweli tumemsikia msemaji wa Accacia, Madam Hecter Pendaeli Poya akizungumza na baadhi ya vyomba vya habari akieleza kwamba wamevunja mkataba na akieleza sababu za kuvunja mkataba kwamba ni kutokana na mgogoro usiokwisha ndani ya Accacia Stand United”

Msemaji huyo amekataa ukweli wa kwamba Stand United inakabiliwa na migogoro katika kipindi hiki na kusema kwamba tayari walishafanya uchaguzi uliowaweka madarakani viongozi wao wa sasa.

Kikosi hicho kimeshuka dimbani mara mbili na kujikusanyia pointi mbili kufuatia sare mbili mfululizo huku ikijiandaa kutupa karata yake nyingine Jumamosi hii dhidi ya Toto Africa.

TPBC Yawataka Wadau Wake Kufuata Taratibu Na Sheria
Daniel Amoah Aanza Mazoezi Azam FC