Uongozi wa Stand Utd umejizatiti kukiwezesha kikosi chao kufanya vyema katika michezo miwili ya ligi kuu ya soka Tanzania bara itakayowakabili kabla ya kufungwa kwa pazia la msimu huu itakapofika Mei 21.
Stand Utd watacheza dhidi ya Simba SC na kisha kufunga msimu dhidi ya Ruvu Shooting katika miji ya Dar es salaam na Pwani.
Afisa habari wa Stand Utd Deo Kaji Makomba amesema mikakati iliyopangwa na uongozi wa juu ni kabambe, na wanaamini itasaidia kufikia lengo la kuzinyakua point sita ambazo zitawahakikishia kusalia katika ligi kuu.
Deo Kaji amesema tayari kikosi chao kipo katika maandalizi ya kuikabili michezo hiyo miwiwli ambayo amekiri itakua migumu kwao kutokana na uhitaji wa point tatu muhimu.
“Kwa kuonyesha ni vipi tupo katika harakati nzuri na kuhakikisha tunapambana katika michezo dhidi ya Simba SC na Ruvu Shooting, tumeshacheza michezo ya kirafiki mjini Kahama na tumepata taswira nzuri ya kuyatambua mapungufu ambayo yanaendelea kufanyiwa kazi na benchi la ufundi katika kipindi hiki.”
“Tunajua uhalali na umuhimu wa michezo yetu miwili iliyosalia, na hatutaki kufanya mzaha ambao utapelekea kupoteza michezo hii, na ikitokea tunapoteza huenda mambo yakawa mgumu sana kwetu.” Amesema Makomba.
Stand Utd ipo katika nafasi ya 6 kwenye msimamo wa ligi kuu ya soka Tanzania bara kwa kufikisha point 35, huku ikikabiliwa na changamoto ya kuvutwa shati na timu zinazowania kubaki ligi kuu kwa kuepuka janga la kushuka daraja.