Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),  Selemani Jafo ameelekeza Uongozi wa Mkoa wa Dar es salaam kuhakikisha Stendi Mpya ya Mabasi ya Mbezi Luis inaanza kutumika muda wowote kuanzia sasa baada ya kujiridhisha kukamilika kwa miundombinu yote muhimu kasoro Barabara ya kuingia kituoni hapo ambayo ipo hatua ya mwisho.

Waziri Jafo amesema hayo wakati alipofanya ziara katika stendi hiyo ambapo amesema muda wowote ambao wakala wa barabara TANROAD watathibitisha kuwa barabara ya kuingia kituoni hapo imekamilika ni vyema kituo kitaanza kutoa huduma.

Aidha Waziri Jafo amesema kutokana na Stendi hiyo kuwa na hadhi ya kimataifa anapendekeza ipewe jina la Rais Dkt. John Magufuli Kama sehemu ya shukrani na kuthamini jitiada alizofanya ambapo amesema atamuomba  Rais Magufuli aridhie ombi hilo.

Hata hivyo, Waziri Jafo amemuelekeza Mkandarasi anaejenga eneo la maegesho ya magari madogo kuhakikisha anakamilisha kazi ndani ya wiki mbili kuanzia leo huku akitaka taa zifungwe ndani ya wiki moja kuanzia leo.

Pamoja na hayo Waziri Jafo ametoa pongezi kwa uongozi wa Mkoa wa Dar es salaam kwa usimamizi madhubuti uliosaidia Stendi hiyo kukamilika ikiwa na ubora uliokusudiwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji la Dar es salaam Bi.Spora Liana amesema kazi zinazoendelea kwa Sasa ni ufungaji wa viyoyozi, lifti, ufungaji wa taa na vifaa vya matangazo, uunganishwaji wa maji kwenye Vyoo na miundombinu mingine ambayo nayo ipo hatua ya mwisho kukamilika na kusisitiza kuwa kwa Sasa Stendi inaweza kuanza kutumika.

Senzo: Kuna mavuvuzela hapa Tanzania
Thomas Tuchel akabidhiwa 'FUPA' lililomshinda Lampard