Uongozi wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Young Africans umesema unafanya mchakato ili kuhakikisha mchezaji wao Stephane Aziz Ki anarejea nchini mapema kuungana na wenzake kujiandaa na mchezo wa Raundi ya Kwanza wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Al Merreikh ya Sudan.
Mchakato huo unafanyika kwa kushirikiana na Shirikisho la Soka nchini Burkina Faso.
Kumekuwa na hofu kwamba mhezaji huyo huenda akachelewa kurejea nchini kutoka Morocco alikokuwa na timu yake ya taifa ya Burkina Faso kwa ajili ya mchezo wao wa mwisho wa kufuzu fainali za AFCON dhidi ya Sudan Kusini kutokana na tetemeko kubwa la ardhi lililotokea katika jiji la Marrakech, Morocco na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 2,000.
Akizungumza jijini Dar es salaam, Afisa Habari wa miamba hiyo ya soka Tanzania Bara Ally Kamwe amesema baada ya tukio hilo klabu imefanya jitihada za kujua taarifa za mchezaji huyo na wameambiwa yupo salama na sasa wanafanya mchakato wa kumrudisha nchini aweze kuungana na wenzake kujiandaa na mchezo wao wa Septemba 16 dhidi ya Al Merreikh.
“Baada ya kujua kwamba mchezaji wetu Aziz Ki yupo salama jitihada tunazozifanya kwa sasa kama klabu inayommiliki ni kuzungumza na Shirikisho la soka la Burkina Faso ambalo Aziz yupo chini yake kwa sasa ili kumsafirisha aweze kuwahi maandalizi ya mchezo wetu wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AI Merreikh tutakaocheza Rwanda Septemba 16,” amesema Kamwe.
Meneja huyo wa Habari amesema mbali na Aziz Ki wachezaji wengine waliokuwa kwenye timu zao za taifa hasa wale waliokuwepo Taifa Stars, wanatarajia kuingia kambini na wenzao leo Jumatatu (Septemba 11) huku Mlinda Lango Djigui Diarra na kiungo Khalid Aucho wakitarajiwa kujiunga na wenzao kesho Jumanne (Septemba 12).
Aidha, Kamwe amesema maandalizi ya timu yao kuelekea Kigali Rwanda yanakwenda vizuri na tayari uongozi umetanguliza watu maalumu kwa ajili ya kuandaa sehemu nzuri ambapo timu yao itafikia kujandaa na mchezo huo ambao wameupa uzito mkubwa
Msafara wa Young Africans unatarajia kuondoka nchini Septenba 14 ukiwa na wachezaj 24 kwa ali ya mchezo huo ambao Kocha Mkuu Miguel Gamondi ameahidi kupata shindi ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kutingga hatua ya makundi ya michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika