Mshambuliaji wa zamani wa klabu ya Namungo FC Stephen Sey yupo huru kuitumikia klabu yoyote Duniani, kufuatia kesi yake kutolewa maamuzi na Shiriklisho la Soka Duniani ‘FIFA’.
Mshambuliaji huyo kutoka nchini Ghana, ambaye kwa sasa yupo nchini Tanzania, aliingia kwenye mzozo wa kimaslahi na klabu ya Eastern Company Sporting Club ya nchini Misri, hali ambayo ilimsukuma kufungua kesi FIFA akidai fidia ya kuvunjwa kwa mkataba wake.
Mshambuliaji huyo ambaye pia amecheza soka katika klabu ya Singida United, amezungumza na Dar24 na kueleza namna alivyopokea hukumu ya FIFA, ambayo imeitaka klabu ya Eastern Company Sporting Club kumlipa kiasi cha pesa ambacho hakuwa tayari kukianika hadharani.
“Ninajihisi furaha kwa hukumu ya kesi yangu kutangazwa, sasa nipo huru kujiunga na klabu yoyote hapa Tanzania ama sehemu nyingine yoyote.”
“Sipo tayari kutaja kiasi gani ambacho Eastern Company Sporting Club wametakiwa kunilipa, lakini ninataka ifahamike wazi kuwa hukumu imetangazwa na nimeshinda dhidi yao.” amesema Sey
Hivi karibuni zilisambaa picha zikimuonesha amevaa jezi ya Geita Gold huku wadau wa michezo wakiamini huenda angetua kwa wachimba madini hao wa Geita lakini dili hilo lilishindikana kutokana na sakata lake hilo kuendelea.
Sakata la Sey na klabu ya Eastern Company Sporting Club inakua ni muendelezo wa taarifa mbaya kwa klabu za kaskazini mwa Barani Afrika dhidi ya baadhi ya wachezaji waliowahi kucheza soka la Bongo, ambao waliwahi kupata dili la kutimkia kwenye nchi za ukanda huo.
Hapa Tanzania tatizo kama hilo limewahi kuwakuta viungo washambuliaji Simon Msuva na Shiza Ramadhan Kichuya.