Mshambuliaji kutoka nchini Ghana na klabu ya Namungo FC Stephen Sey huenda akaibukia Azam FC, kufautia kiwango chake kumkuna kocha mkuu wa klabu hiyo George Lwandamina.
Sey alionesha kiwango kizuri kwenye mchezo wa Ligi Kuu kati ya Namungo FC dhidi ya Azam FC uliochezwa jana Jumatatu usiku, Uwanja wa Azam Complex Chamazi.
Tetesi zinaeleza kuwa kiwango cha mshambuliaji huyo aliejiunga na Namungo FC akitokea Singida United, kimemvutia Lwandamina, ambaye amedhamiria kufanya maboresho kwenye kikosi cha Azam FC.
Kocha huyo kutoka nchini Zambia amepanga kufanya hivyo katika kipindi cha dirisha dogo la usajili ambalo litafunguliwa rasmi kesho Jumatano (Desemba 16).
Hivi karibuni Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino Azam FC Thabit Zakaria aliweka wazi kwamba kuna mpango wa kufanya usajili kwenye dirisha dogo, ambalo linatarajiwa kufunguliwa kesho Desemba 16, ikiwa kutakuwa na mapendekezo ya benchi la ufundi.
“Usajili ni kwa ajili ya timu kubwa nasi pia lazima tufanye usajili kutokana na mapendekezo ya mwalimu.” alisema Thabit.
Sey alifunga bao la kufutia machozi upande wa Namungo FC dhidi ya Azam FC ambao walitangulia kupata mabao la mawili ya kuongoza yaliyofungwa na Iddy Seleman ‘Naldo’. Edward Charkes Manyama aliifungia nNamungo FC bao la kwanza.
Kwa matokeo hayo Azam FC wanafikisha alama 28, ambazo zinaendelea kuwaweka kwenye nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu, wakitanguliwa na mabingwa watetezi Simba SC wenye alama 29, huku Young Africans wakiongoza kwa kuwa na alama 36.