Mshambuliaji wa pembeni kutoka nchini England na klabu ya Manchester City Raheem Shaquille Sterling, ametangaza matarajio ya mafanikio ya klabu hiyo kwa msimu ujao wa 2017/18.
Starling amesema matarajio yake makubwa ni kuona klabu ya Man city inatwaa ubingwa, kutokana na mipango inayoendelea kufanywa na meneja wake Pep Guardiola.
Mshambuliaji huyo ambaye alijiunga na Man City akitokea Liverpool mwaka 2015, amesema mipango ya usajili ndio inayompa jeuri ya kuamini msimu ujao ubingwa wa PL utaelekea Etihad Stadium, bila kipingamizi chochote.
“Tunahitaji kutwaa ubingwa wa ligi ya England msimu ujao,” amesema mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 22 alipohojiwa na tovuti ya Man City FC (www.mancity.com).
“Kwangu litakua jambo la kujivunia sana, kwa sababu nina hamu kubwa ya kujipa heshima ya kuwa bingwa kwa kushirikiana na wachezaji wenzangu, kikosi kinaendelea kuimarika kutokana na uweledi wa meneja wetu. Hivyo sina shaka na mambo mazuri tutakayo yafanya kwa msimu ujao.”
Msimu uliopita Man City walishindwa kufikia lengo la kutwaa ubingwa wa England kwa kuachwa nyuma kwa point 15 dhidi ya mabingwa Chelsea.
Kwa mara ya mwisho Man city walitwaa ubingwa wa England mwaka 2014, walipokua wakinolewa na meneja kutoka nchini Chile Manuel Pellegrini.
Mpaka sasa klabu hiyo imeshakamilisha usajili wa mlinda mlango Ederson aliyetokea SL Benfica ya Ureno kwa ada ya Pauni milioni 34.7 sawa na dola za kimarekani milioni 44.92,kiungo Bernardo Silva aliyetokea AS Monaco ya Ufaransa kwa ada ya Pauni milioni 43 pamoja na beki wa kulia Kyle Walker aliyetokea Spurs kwa ada ya Pauni milioni 50.
Man City watacheza mchezo wa kwanza wa kirafiki ambao ni sehemu ya kujiandaa na msimu mpya wa ligi dhidi ya mahasimu wao Manchester United huko nchini Marekani siku ya Alkhamis.
Man City pia watapambana na mabingwa wa soka nchini Hispania Real Madrid pamoja na makamu bingwa wa ligi ya England Tottenham Hotspur.
Timu hizo zitakutana katika michuano ya International Champions Cup.