Aliyekua nahodha na kiungo wa majogoo wa jiji (Liverpool) Steven George Gerrard, ametajwa kuwa miongoni mwa mameneja wanaowania kiti cha ukuu wa benchi la ufundi la klabu ya Rangers ya nchini Scotland.
Tovuti ya The Guardian na BBC Sport zimetoa taarifa za kiungo huyo aliyecheza Liverpool kwa mafanikio makubwa kuanzia mwaka 1982-2015, anajadiliwa na bodi ya klabu ya Rangers ambayo inaendelea kumsaka atakaepewa jukumu la kukiongoza kikosi chao.
Kikosi cha Rangers kwa sasa kinanolewa na meneja wa muda Graeme Murty, baada ya kutimuliwa kwa Pedro Caixinha mwezi Oktoba mwaka 2017.
Mwenyekiti wa klabu ya Rangers Dave King alionekana Anfield siku ya jumanne usiku wakati wa mchezo wa mkondo wa kwanza wa nusu fainali kati ya Liverpool dhidi ya AS Roma, jambo ambalo linatajwa kuwa moja ya mikakati ya kiongozi huyo kuzungumza na Gerrard.
Mbali na hatua hiyo, Gerrard naye alionekana nchini Scotland mwishoni mwa juma lililopita akishuhudia mpambano wa Rangers ambao walikubali kupoteza dhidi ya mahasimu wao wakubwa Celtic kwa idadi ya mabao matatu kwa mawili.
Gerrard ambaye aliwahi kuwa nahodha wa timu ya taifa ya England alitangaza kustaafu soka mwaka 2016, na baadae alianza kujishughulisha na tasnia ya ukufunzi. Kwa sasa anakinoa kikosi cha vijana chini ya miaka 18 cha Liverpool. Hajawahi kuwa meneja wa timu yoyote ya wakubwa katika ngazi ya klabu.
Kama Gerrard atakabidhiwa jukumu la kuwa meneja wa klabu ya Rangers, atakua na kazi nzito ya kukabiliana na aliyewahi kuwa bosi wake akiwa Liverpool Brendan Rodgers, ambaye yupo upande wa mawasimu Celtic.
Rangers inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi nchini Scotland, ikiwa nyuma kwa alama kumi dhidi ya Caletic, na imesaliwa na michezo minne.