Kocha wa Azam FC, Stewart Hall, amesema kuwa mabadiliko aliyofanya kipindi cha pili kwa kiasi kikubwa yamechangia ushindi wa mabao 2-1 walioupata dhidi ya Esperance ya Tunisia.

Mchezo huo wa raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika ulifanyika kwenye Uwanja wa Azam Complex jana jioni, mabao ya Azam FC yalifungwa na viungo washambuliaji Farid Mussa na Ramadhan Singano ‘Messi’.

Mabadiliko hayo ni ya kuwaingiza Frank Domayo na Khamis Mcha kipindi cha pili, ambao walichukua nafasi za Michael Bolou na Waziri Salum.

Akizungumza jana, Hall alisema alitumia mifumo miwili tofauti kwenye mchezo huo, mfumo mpya kuwahi kuutumia msimu huu wa 4-4-3 na baadaye kurejea katika mfumo wake wa kawaida wa 3-5-2 mara baada ya kumtoa Wazir Salum.

“Nimelazimika kutumia mfumo wa 4-3-3 leo (jana) baada ya kumkosa beki Shomari Kapombe ambaye ni mgonjwa, mfumo huo umefanya kazi baada ya kupata bao moja na pia bao la pili lilipatikana baada ya kutumia 3-5-2.

“Baada ya kutoka Wazir nililazimika kubadilisha mfumo kutoka 4-3-3 hadi 3-5-2, hii ilitufanya tuzidi kucheza vema kwani mara baada ya kumpleka Messi pembeni kutoka namba nane alicheza vizuri na hata Farid naye alikuwa vizuri, hii pia ilitoa nafasi kwa Mcha (Khamis) kucheza namba 10, pia kuingia kwa Domayo kipindi cha pili kulituongezea kasi na kupata mabao hayo,” alisema.

Hall alisema walitengeneza nafasi nyingi kipindi cha kwanza na kusindwa kuzitumia vema, lakini amejipa matumaini zaidi kwa kueleza kuwa kikosi chake bado kinanafasi ya kusonga mbele katika mchezo wa marudiano jijini Tunis, licha ya kuruhusu bao moja nyumbani.

Timu hizo zinatarajia kurudiana Aprili 20 mwaka huu kwenye Uwanja wa Rades mjini Tunis, na Azam FC inatakiwa ipate sare ya aina yoyote au ushindi ili iweze kusonga mbele kwa raundi ya mwisho ya mtoano (play off) kwa kukipiga na timu iliyoteremka kutoka Ligi ya Mabingwa Afrika na mshindi wa jumla atasonga mbele kwa hatua ya makundi.

Kocha Mayanja Amfukuza Kambini Hamisi Kiiza
Wabunge warudia maswali ya Lowassa kuhusu Uamuzi wa Magufuli kwenye fedha