Kocha mkuu wa timu ya taifa Afrika kusini Stuart Baxter amewashangaza mashabiki wa soka nchini humo kwa kumuita kiungo Thulani Serero, kwenye kikosi kitakachoikabili Nigeria, katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Afrika 2019 mwezi huu.
Serero anaeitumikia klabu ya Vitesse Arnhem ya Uholanzi, mwaka 2017 aliwahi kumwambia kocha huyo wa Bafana Bafana, hatokua tayari kuitikia wito wake kama hatohakikishiwa kucheza kwenye kikosi cha kwanza.
“Sofa za Arnhem zina burudani zaidi kuliko benchi la timu ya taifa ya Afrika kusini. Kama timu ya taifa inanihitaji, ni lazima wanihakikishie nitacheza kwenye kikosi cha kwanza,” ni kauli aliyoitoa Serero kabla ya mchezo wa kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia 2018, mwezi Novemba 2017 dhidi ya Senegal.
Kocha Baxter amesema ameona kuna umuhimu wa kumuita kiungo huyo, kutokana na umuhimu wa kuhitaji kushinda mchezo dhidi ya Nigenia, na tayari amemuhakikishia atamuanzisha kwenye kikosi cha kwanza.
“Tunahitaji kucheza soka la kushambulia, tunahitaji kushinda mchezo wetu na Nigeria, nimeona kuna umuhimu wa kumuita Serero, ninaamini atatusaidia katika mipango yetu,”
Kocha mkuu wa timu ya taifa Afrika kusini Stuart Baxter.
“Nimeongea naye na nimemueleza umuhimu wa mchezo wetu dhidi ya Nigeria, ninaamini atakua sehemu ya kikosi, ambacho kitakua na kazi ya kushinda katika ardhi ya nyumbani.” Alisema kocha Baxter.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 28, anatarajiwa na wengi huenda akawa amebadilika kitabia na atakua tayari kurejea Afrika kusini kwa ajili ya mchezo dhidi ya Nigeria, ambao ni muhimu kwa Bafana Bafana kupata ushindi.
Katika hatua nyingine kocha Baxter anakabiliwa na changamoto ya wachezaji wake muhimu kuwa majeruhi hususan wanaocheza kwenye nafasi ya kiungo Dean Furman, Kamohelo Mokotjo na Bongani, hivyo hakua na njia mbadala zaidi ya kumuita Serero.
Kikosi kamili kilichotajwa kwa ajili ya mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Afrika 2019 dhidi ya Nigeria, utakaounguruma Novemba 17 kwenye uwanja wa Soccer City.
MAKIPA: Darren Keet (Bidvest Wits), Itumeleng Khune (Kaizer Chiefs) na Ronwen Williams (SuperSport United),
MABEKI: Thulani Hlatshwayo, Sifiso Hlanti (both BidVest Wits), Motjeka Madisha (Mamelodi Sundowns), Innocent Maela (Orlando Pirates), Thamsanqa Mkhize (Cape Town City), Buhle Mkhwanazi (BidVest Wits), Ramahlwe Mphahlele (Kaizer Chiefs) na Siyanda Xulu (Maritzburg United)
VIUNGO: Hlompho Kekana (Mamelodi Sundowns), Thembinkosi Lorch (Orlando Pirates), Lebohang Maboe, Tiyani Mabunda (Mamelodi Sundowns), Fortune Makaringe (Maritzburg United), Teboho Mokoena (SuperSport United), Vincent Pule (Orlando Pirates), Thulani Serero (Vitesse Arnhem, Netherlands) na Themba Zwane (Mamelodi Sundowns)
WASHAMBULIAJI: Lebo Mothiba (Racing Strasbourg, France), Dino Ndlovu (Hangzhou Greentown, China) na Percy Tau (Royal Union St Gilloise, Belgium).