Wasanii wa kizazi kipya Aslay na Nandy hatiani kupelekwa mahakamani kwa tuhuma za kufanyia kazi wimbo ujulikanao kama ”Subalkheri” ulioimbwa na kikundi cha Taarabu Asilia visiwani Zanzibar (Culture Music Club) bila ridhaa toka kwa kikundi hiko.
Hayo yameibuka mara baada wasanii hao kutuhumiwa kutoa kiasi kidogo cha fedha laki nane, 800,000 na kuwalipa baadhi ya wasanii katika kundi kama namna ya kufidia kazi hiyo kitendo ambacho ni ukiukaji wa katiba ya kikundi hicho.
Hivyo imedaiwa kuwa wamevunja katiba ya kikundi ibara ya Sita (6) inayosema kuwa nyimbo zote zilizoimbwa na kikundi ni mali ya kikundi na kwamba muimbaji, mtunzi na muweka sauti watakuwa na haki zao kupitia kikundi hicho kwa kuwalipa baadhi ya waimbaji wa wimbo huo.
“Walichokifanya Aslay na Nandy kwenda kwa waimbaji wetu na kuwapa kiwango hicho cha fedha kwetu tunaona hakikubaliki na wametoa kama zawadi tu kwa sababu thamani ya wimbo wetu haulingani na kiwango hicho. Kwa mujibu wa katiba ya kikundi chetu, ibara ya sita inaeleza nyimbo zote zilizoimbwa na kikundi ni mali ya kikundi na kwamba muimbaji, mtunzi na muweka sauti watakuwa na haki zao kupitia kikundi hicho”, amesema Twaha.
Hata hivyo Katibu Mtendaji wa Kikundi hicho Taimur Rukuni Twaha amesema kitendo cha wasanii hao kuimba wimbo huo Subalkheri bila ridhaa sio sawa na ilitakiwa wasanii hao kuonana na uongozi ili kufanya makubaliano.
Hivyo kama kikundi hawazitambui pesa hizo kwani hazijitoshelezi kufidia thamani ya wimbo huo na wamejipanga kulifikisha swala hilo mbele ya mahakama ili waweze kupata haki yao.
Kwa upande mwingine, Twaha amesema msimamo wao utabaki pale pale wa kuwafikisha Mahakamani wasanii hao endapo watashindwa kutimiza masharti waliyopewa na uongozi wa kikundi hicho.