Rais wa Marekani Donald Trump amesema Sudan itaondolewa kwenye orodha ya mataifa yanayofadhili makundi ya kigaidi, ikiwa itakubali kutoa jumla ya dola milioni 335 kuwalipa wahanga wa Kimarekani wa mashambulizi ya kigaidi pamoja na familia zao.
“Habari njema! Serikali mpya ya Sudan, ambayo inafanya maendeleo ya kweli, imekubali kulipa dola milioni 335 kama fidia kwa wahanga wa Marekani wa ugaidi na familia zao, mara baada ya kulipwa, nitaiondoa Sudan kwenye orodha ya mataifa yanayofadhili ugaidi, ” ameandika Trump kwenye ukurasa wake wa Twitter.
Muda mfupi baada ya tangazo la Trump, Waziri Mkuu wa Sudan, Abdalla Hamdok amejibu kwa kusema kuwa tayari fedha hizo zimehamishwa, na wanasubiri uthibitisho kutoka kwa mamlaka ya Marekani.
Hatua inatarajiwa kufungua milango kwa nchi hiyo kupata mikopo ya kimataifa na misaada inayohitajika kufufua uchumi wake ulioporomoka pamoja na kuisaidia nchi hiyo kuwa ya kidemokrasia.
Trump ametoa tamko hilo zikiwa zimebaki takriban wiki mbili hadi siku ya uchaguzi mkuu wa Marekani.
Marekani ilichukua uamuzi wa kuiweka Sudan katika orodha hiyo mnamo mwaka 1993, ikiamini rais wa Sudan wa wakati huo, Omar al-Bashir alikuwa akifadhili makundi ya kigaidi.