Sudan imetangaza miezi mitatu ya hali ya dharura nchini kote, kufuatia mafuriko ambayo yamesababisha vifo vya watu 100, pamoja na kuathiri nyumba 100,000.
Wizara ya mambo ya ndani nchini humo imesema kupitia mtandao wa kijamii. Kulingana na shirika la habari linalomilikiwa na serikali nchini humo SUNA, limeripoti mafuriko hayo ambayo pia yamewajeruhi watu 46, ni miongoni mwa majanga mabaya zaidi ya asili kuwahi kulikumba taifa hilo baada ya miongo mingi.
Darfur kaskazini iliyoko magharibi mwa nchi hiyo pamoja na jimbo la Sennar lililoko kusini mwa Sudan, ni miongoni mwa maeneo ambayo yameathiriwa zaidi.
Ripoti ya hivi karibuni kutoka katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu masuala ya kiutu, mnamo siku ya Alhamisi, ilisema tayari watu 380,000 wameshaathiriwa na mafuriko mwaka huu.