Imefahamika kuwa Uongozi wa Chama cha Soka nchini Sudan ‘S.F.A’, umewasilisha ombi la kutaka kuwa mwenyeji wa Michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati ‘CECAFA Kagame Cup 2023’.
S.F.A imewasilisha ombi hilo, huku ikithibitika tayari nchi za Rwanda na Tanzania zimeonesha nia ya kutaka kuwa mwenyeji wa Michuano hiyo ambayo kwa mara ya mwisho ilifanyika jijini Dar es salaam mwaka 2021.
Hata hivyo CECAFA inatarajiwa kutoa jibu la nani atakuwa mwenyeji wa Michuano hiyo mwaka 2023, baada ya Kamati ya Utendaji kufanya maamuzi katika kikao maalum kitakachofanyika siku za karibuni.
Michuano ya Mwaka huu 2023 inatarajiwa kuanza kati ya Julai 15 hadi 29 kwa kushiriki timu bingwa za mataifa ya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Klabu ya Express ya Uganda ndio Bingwa mtetezi wa Michuano hiyo baada ya kuifunga Nyasa Big Bullets ya Malawi bao 1-0, katika mchezo wa Fainali mwaka 2021, jijini Dar es salaam.