Khartoum, Sudan Viongozi wa mlengo wa mabadiliko nchini Sudan wamejibu hotuba ya mkuu mpya wa Baraza la Mpito la Kijeshi la nchi hiyo na kuonya kuhusu kudharauliwa matakwa ya wananchi.

Harakati ya Taifa ya Mabadiliko (NFC) ambayo ni muungano wa vyama mbalimbali vya upinzani vya kisiasa na vya ushirika vya Sudan umetoa taarifa rasmi ukigusia hotuba ya Luteni Jenerali Abdel Fattah Abdelrahman Burhan, Mkuu wa Baraza la Mpito la Kijeshi la Sudan na kusema kuwa, hotuba yake haikutoa majibu ya matakwa yeyote kwa wananchi, hivyo wataendelea na maandamano na mgomo mpaka watakapotekelezewa matakwa yao.

Wapinzani nchini Sudan wametoa masharti mengine kadhaa ikiwa ni pamoja na kubadilishwa muundo wa taasisi za kiusalama pamoja na kuvunjwa vikosi vyote vya wanamgambo wa utawala uliopinduliwa wa Jenerali Omar al Bashir vikiwemo vikosi vya ulinzi wa raia na polisi jamii.

Taarifa ya harakati hiyo imeongeza kuwa, vikosi vyote fisadi katika majeshi ya Sudan vimefanya uhalifu mkubwa katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo hasa Darfur. Jibal al Nouba, Kusini mwa Nile na maeneo mengine ya nchi hiyo, hivyo wahusika wote lazima wapandishwe kizimbani.

Sudan imekumbwa na maandamano makubwa ya wananchi tangu tangu tarehe 19 Disemba 2018 kupinga utawala wa miaka 30 wa Jenerali Omar al Bashir.

Alhamisi iliyopita, jeshi la Sudan lilifanya mapinduzi ya kijeshi yaliyomng’oa madarakani al Bashir. Hata hivyo wapinzani wanaendelea na maandamano wakisema huo ni mchezo tu wa kisiasa wa kuvunja nguvu matakwa ya wananchi.

Rais Tshisekedi aanza ziara ya ndani, azuru Kivu Kaskazini
Aliyeiba kichanga wa siku moja akamatwa, alitumia mbinu hii...