Baadhi ya familia na jamaa za watu waliouawa katika mapigano nchini Sudan wamesema wamekuwa wakitumia muda wa utulivu (usio wa mapigano), kuzika miili ya jamaa zao zilizohifadhiwa katika hospitali ya jijini Khartoum.
Raia hao, wamesema hata hivyo utulivu huo ni wa nadra kwani mapigano makali na milio ya risasi vimeendelea kushuhudiwa baada ya muda wa sitisho la mapigano la saa 24 kumalizika.
Bado Mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan na makamu wake wa zamani Mohamed Hamdan Dagalo, anayeongoza kikosi cha kijeshi cha Rapid Support Forces, wanaendelea kushambuliana.
Mfululizo wa makubaliano ya hivi karibuni ya kusitisha mapigano yaliwawezesha raia waliokwama katika mji mkuu wa Khartoum kwenda nje kukusanya chakula na mahitaji mengine muhimu lakini hali hiyo sasa haipo.