Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph ‘Sugu’ Mbilinyi amesimulia baadhi ya mambo aliyoyaandika kwenye historia yake alipokuwa amefungwa gerezani mjini humo.
Sugu ambaye aliachiwa huru pamoja na Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Kanda ya Nyasa, Emmanuel Masonga kwa msamaha wa Rais John Magufuli alioutoa siku ya maadhimisho ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, amesema kuwa alipoingia gerezani siku ya kwanza, wafungwa walipata mshtuko kumuona.
“Kwanza wafungwa walishtuka kuniona na isingekuwa kujishusha ilitaka kutokea vurugu mle ndani,” Sugu anakaririwa kwenye mahojiano maalum na Mwananchi. “Lakini nilikaa nao nikawaambia kwanini niko mle ndani na nikawaambia ‘msiogope ndiko nchi ilipofika kwa sasa’, wakanielewa na maisha yakaendelea,” aliongeza.
Aidha, Sugu anasema kuwa mbali na wafungwa, zaidi ya asilimia 90 ya askari magereza walionesha kumheshimu na hata kuendelea kumuita ‘mheshimiwa’ wakati wote alipokuwa ndani.
“Yaani mle ndani ni kama vile kulikuwa na jimbo ndani ya gereza, muda wote niliokaa gerezani na wafungwa wenzangu niliitwa mheshimiwa na sio jina lingine,” alisema na kuongeza kuwa ni kama kulikuwa na jimbo lingine ndani ya gereza hilo.
Aliongeza kuwa alikuwa anazungumza na askari wa gereza hilo ambao walikuwa wanamueleza changamoto zao kama wapiga kura wake wakimtaka kufahamu kuwa wanachofanya ni kutimiza majukumu yao kwani sio wao waliompeleka gerezani.
Februari 26, Sugu na Masonga walihukumiwa kifungo cha miezi mitano walipokutwa na hatia ya kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli. Waliachiwa huru Mei 10 kwa msamaha wa Rais.