Mbunge wa jimbo la Kawe Chadema Halima Mdee amefunguka kuhusiana na kitendo cha Mahakama kumnyima dhamana Mbunge wa Mbeya mjini, Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu anayeshikiliwa na polisi kwa kesi ya kufanya mkutano wa hadhara na kuongea maneno ya uchochezi dhidi ya Rais.
Mdee amelaumu vikali mahakama kuzuia dhamana hiyo kwani kosa hilo linastahili dhamana kisheria, na kwa taratibu za kisheria ni haki mtuhumiwa kupata dhamana na ni wajibu wa polisi kutoa dhamana.
“Ni zaidi ya wiki sasa Mhe. Sugu yupo ndani lakini amenyimwa dhamana kwa kosa ambalo linadhaminika kisheria” amesema Mdee.
Hivyo ameiomba mahakama kufanya kazi zake kwa haki na si kisiasa kwani anaamini kuwa mahakama ni sehemu pekee tegemezi kwa wananchi wanyonge.
Aidha amemuomba Jaji Mkuu Prof. Ibrahim Hamis Juma kufuatilia mwenendo wa kesi za kisiasa nchini na kudai kuwa baadhi ya mahakimu wamekuwa wakipindisha mambo kwa sababu za kisiasa.
Jaji Mkuu na yeye anapaswa kuyatambua haya na kuwakemea baadhi ya Mahakimu ambao wanafanya vitu kama hivi” alisema Mdee.
Mbali na hilo Halima Mdee amedai kuwa kuna tetesi za kutaka kumfunga Mbunge wa Mbeya Mjini Mhe. Joseph Mbilinyi “Sugu’ kama ambavyo alifungwa Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali.