Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei amethibitisha jeshi hilo kumuita Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA), Joseph Mbilinyi kwa kile walichokisema kuwa Mbunge huyo ametoa kauli ya uchochezi juu ya zoezi la kugawa vitambulisho kwa wafanyabiashara wadogo.
Kwa mujibu wa Kamanda Matei, zoezi la kugawa vitambulisho lilikuwa na lengo zuri la kuwatambua wafanyabiashara hao lakini Mbunge huyo ameonekana kulikosoa kwa kutoa maneno ambayo yaliyoashiria uchochezi.
“Ni kweli tumemuita Mbunge Joseph Mbilinyi kwa mahojiano kutokana na maneno yake aliyoyazungumza kuhusu vitambulisho, maana tunaona kuna kukashifu, vile ni vitambulisho vilivyotolewa na serikali sasa tunapoona mtu anaanza kutoa maneno hayo, huo ni uchochezi,”amesema Matei
Aidha, mapema wiki hii Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila alibainisha juu ya uwepo wa baadhi ya kauli zilizoashiria kudharau tukio la kugawa vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo wadogo ikiwa ni agizo la Rais Magufuli.
Hata hivyo, Disemba 2018 Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliwakabidhi Wakuu wa Mikoa vitambulisho maalum kwa ajili ya kuvigawa kwa wafanyabiashara wadogo ili waweze kutambulika.