Katika kuhakikisha kuwa kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli ya kuibadili nchi kuwa ya viwanda, Shirika la uzalishaji mali za Jeshi la kujenga Taifa (JKT) limeunga mkono kauli hiyo kwa kuanza mipango ya kufungua kiwanda cha kusindika minofu.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Suma JKT, Bregadia Jenerali Charo Yateri ambapo amesema kuwa shirika hilo limedhamiria kutoa mafunzo kwa vijana kupitia miradi mbalimbali ambayo ipo chini ya shirika hilo.
“SUMA JKT imeendelea kujiimarisha kupitia miradi yake ya kilimo, huduma za ulinzi, uvuvi pamoja na ufugaji, ambapo ina viwanda vya kusindika na kuchakata mazao, na asali ambapo kupitia miradi na viwanda hivyo imetoa ajira 4,500 kwa vijana nchini ,hivyo kwa sasa tunajipanga kuanzisha kiwanda hicho,” amesema Brigedia Jenerali Yateri
Aidha, Brigedia Jenerali Yateri amesema SUMA JKT inajivunia miradi hiyo sambamba na kuwa na kilimo cha mazao ya biashara kama vile kahawa mkoani Mbeya na mchikichi mkoani Kigoma, sambasamba na uwezo wa kujitegemea kwa asilimia 55, huku ikipata ruzuku ya serikali asilimia 45 tu.
Hata hivyo, Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA JKT), lilianzishwa mwaka 1982, kwa tamko la Rais chini ya sheria ya uanzishaji wa mashirika ya umma kwa lengo la kuisaidia serikali kupunguza gharama za kuendesha mafunzo kwa vijana wanaopatiwa ujuzi wa aina mbalimbali.