Jumla ya Vijana 6,000 kutoka Jeshi la Wananchi Tanzania – JWTZ, (Suma JKT) wameanza kuwasili Wilayani Handeni Mkoani Tanga, kwa ajili ya shughuli ya ujenzi unaotarajia kutumia Shilingi 97 Bilioni wa nyumba 5,000 za kijiji cha Msomera zitakazotumiwa na Wananchi watakaohamia kwa hiari kutoka Ngorongoro.
Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa – JKT, Meja Jenerali Rajabu Mabele amesema Vijana 500 wamesharipoti eneo la mradi na wengine wanaendelea kuingia na kwamba wamepokea fedha kutoka kwa uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro, na muda wa ujenzi ni miezi sita kuanzia Oktoba 2023 hadi Machi 2024.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro, Jenerali Venance Mabeyo amezitaka Wizara za Kisekta kuharakisha ujenzi wa miundombinu katika eneo la mradi kijijini Msomera, ili wahusika waweze kuanza kazi.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Handeni, Albert Msando amesema wanatarajia kusimamia ujenzi huo kwa wakati, ili kuepukana na mabadiliko ya hali ya hewa hasa mvua ambayo inaweza kuleta changamoto katika usafirishaji wa vifaa vya ujenzi.