Waziri Mkuu mstaafu ambaye alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Frederick Sumaye ametangaza kujiondoa rasmi kwenye chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Sumaye ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa chama Kanda ya Pwani amesema kuwa amechukua uamuzi huo kutokana na mambo yanayoendelea ndani ya chama hicho hususan kwenye mchakato wa uchaguzi wa ndani.
Sumaye aligombea nafasi ya Uenyekiti wa Kanda ya Pwani ambapo alikuwa mgombea pekee, lakini alipigiwa kura 48 za hapana kati ya kura zote 76, hivyo matokeo yalifutwa na uchaguzi unapaswa kurudiwa tena.
“Kutokana na hayo nimelazimika, kwa kulazimishwa, kujiondoa Chadema na kuanzia sasa sio mwana Chadema na sijiungi na chama chochote cha siasa. Nitakuwa tayari kutumika na chama chochote ikiwemo Chadema,” amesema Sumaye.
“Ninawapenda sana Chadema, nina imani kubwa sana na ninyi na nawashukuru sana kwa ushirikiano mlionipa. Ninajua wengi wataumia lakini sina jinsi kwani wengi mtaumia kwa viongozi wenu wa Kanda waliofanya haya na mimi nimewasamehe,” aliongeza.
Mwanasiasa huyo mkongwe amempa ujumbe Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akimtaka kuwa makini na watu wanaomzunguka kwani baadhi yao hawana nia njema.
Sumaye ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1995-2005), alijiunga na Chadema akitokea CCM katika harakati za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 siku chache tu baada ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa naye kujiunga na chama hicho na kupewa nafasi ya kugombea urais.