Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye, aligeuka mwiba kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uzinduzi wa kampeni za urais za vyama vinavyounda Ukawa, Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD.

Sumaye ambaye hivi karibuni alitangaza kujiunga na Ukawa kwa lengo la kuwasaidia, alipewa dakika nyingi zaidi kuzungumza mambo mbalimbali ambayo yalikuwa majibu yake kwa tuhuma mbalimbali zilizokuwa zinaelekezwa kwa mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa.

Sumaye alitoa majibu yake kwa kutumia mifano linganifu kwa kashfa ya Richmond iliyosababisha Lowassa kujiuzulu nafasi ya Uwaziri Mkuu akidai kuwa CCM inamuonea mgombea huyo wa Chadema kwa kuwa kuna masakata mengi makubwa ya ufisadi ambayo yaliendelea baadaye ambayo yanatokana na watendaji wa serikali.

“Mheshimiwa Lowassa alitoka kwenye serikali miaka 8 iliyopita, hivi wakati zile twiga zinapandishwa kwenye ndege, Lowassa alikuwepo?” Alihoji Sumaye.

Alitumia mtindo wa swali hilo kuhoji kuhusu suala la wizi wa fedha katika akaunti ya maalum ya Bank Kuu, External Payments Arrears (EPA), ufisadi wa akaunti ya Tegeta Escrow, Upitishwaji wa magunia 18 ya dawa za kulevya katika kiwanja cha ndege nchini na kukamatwa nchini Afrika Kusini yakiwa moja kati ya madai yake.

Sumaye alisisitiza kuwa serikali ya CCM ni dhaifu na kwamba imeshindwa kuwasaidia wananchi masikini huku akiwataka wananchi kumchagua Edward Lowassa ili kuleta mabadiliko hayo.

Akizungumzia suala linalozungumziwa kuhusu afya ya mgombea huyo, Sumaye alisema, “Ikulu hafanya kazi ya kubeba zege, kazi ya rais ni meneja.” Alitumia pia mtindo wa swali kuwahoji wananchi kuhusu viongozi ambao wamekuwa madarakani lakini walipata kusumbuliwa na magonjwa mbalimbali lakini hawakushindwa kuendelea na kazi.
“Ukiwa na umri zaidi ya miaka 50 hauwezi kuwa mzima kwa asilimia 100,” alisikika Sumaye.

 

 

 

“Lowassa Ametuangusha Kwenye Uzinduzi”
Lowassa Aipiku Ahadi Ya Magufuli