Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Pwani, Frederick Sumaye amezungumzia uwezekano wa kurejea katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) kama alivyofanya Edward Lowassa.
Akizungumza muda mfupi baada ya Lowassa ambaye alikuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chadema na Mgombea Urais wa chama hicho mwaka 2015, Sumaye amesema kuwa kwake ni ndoto isiyokuwepo.
Aidha, Sumaye alidai kuwa Lowassa amefanya uamuzi wake binafsi na kwamba yeye ataendelea kuungana na wenzake kujenga chama.
“Kama kaamua acha aende, sisi tunaendelea kujenga chama. Na hicho ulichouliza cha mimi kuhama ni ndoto ambayo haipo,” Sumaye aliliambia Mwananchi.
“Mimi hainipi shida, mtu akiamua kuhama chama na kwenda kingine ni uamuzi wake,” aliongeza.
Lowassa na Sumaye walikuwa mawaziri wakuu wastaafu waliohama CCM na kujiunga na Chadema katika vuguvugu la uchaguzi wa mwaka 2015.
Lowassa aliihama CCM baada ya jina lake kuondolewa na Kamati Kuu ya CCM katika hatua za awali za mchakato wa kuchuja majina ya walioomba kuwania nafasi ya kugombea Urais.
Mwili wa marehemu Ruge Mutahaba wapokelewa jijini Dar
Kutokana na kutoridhishwa na maamuzi hayo, Lowassa alijiunga na Chadema na kupewa nafasi ya kugombea Urais akiungwa mkono na vyama vitano vya upinzani vilivyounda Ukawa.
Alishindwa uchaguzi huo akipata kura takribani milioni sita, rekodi ambayo ilikuwa ya kihistoria kufikiwa na mgombea urais wa upinzani tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini.