Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Fredrick Sumaye ameupongeza uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano kwa hatua mbalimbali za kuleta maendeleo katika nyanja mbalimbali nchini na hususani katika Jiji la Dar es Salaam.
Sumaye ambaye aliwahi kushika wadhifa wa Waziri Mkuu kwa miaka 10 katika utawala wa Serikali ya Awamu ya tatu,
Ameyasema hayo jijini Dar es Salaam mara baada kumalizika kwa uchaguzi uliofanywa na chama hicho na yeye kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kanda hiyo.
“Kwa Dar es Salaam, Serikali imechukua hatua nyingi za kuleta maendeleo, kwa kweli sisi wapinzani inabidi tuwapongeze na kuiunga mkono Serikali hii ya awamu ya tano kwa namna inavyojitahidi kuleta maendeleo natoa wito kwenu tushirikiane nao tuache kugombana nao,”amesema Sumaye.
Aidha, amewaagiza wabunge, mameya, madiwani pamoja na wenyeviti wa mitaa ambao miradi mbalimbali imetekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano kuwaelimisha wananchi namna ya kuwa karibu na miradi hiyo.
Hata hivyo, Sumaye amesema kuwa kazi ya vyama vya upinzani ni kuishauri Serikali iliyoko madarakani na kushirikiana nayo kuleta maendeleo ya nchi.