Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Nigeria, Sunday Oliseh amesema hana budi kuwathibitishia kwa vitendo wadau wa soka nchini humo, wanaobeza uteuzi wake wa kuwa mkuu wa benchi la ufundi la Super Eagles.

Oliseh, mwenye umri wa miaka 40 amekuwa akipokea changamoto za maneno kutoka kwa wadau wa soka nchini Nigeria, kwa wanaodai hana uzoefu wa kufanya kazi ya ukocha katika kikosi chao, hivyo uteuzi wake ni sawa na kazi bure.

Oliseh, ambaye aliwahi kucheza kwenye klabu za Borussia Dortmund na Juventus amesema ni kawaida kwa wadau wa soka kuzungumza lolote kutokana na uhalisia wanaouona kwa macho, na kwake hana budi kuwaonyesha kwa vitendo kama anaweza kufanya kazi ya kuifikisha Nigeruia inapotakiwa kufika.

Oliseh, aliwahi kuwa meneja wa klabu ya Vervietois inayoshiriki madaraja ya nchini humo nchini Ubelgiji, kati ya mwaka 2008 na 2009 na baada ya hapo aliachana na kazi hiyo.

Shughuli nyingine zilizowahi kufanywa na kiungo huyo ambaye alikuwa sehemu ya kikosi cha Nigeria wakati wa fainali za kombe la dunia za mwaka 1994 na 1998 ni kuwa mshauri wa michezo pamoja na mjumbe wa kamati ya ufundi ya shirikisho la soka duniani FIFA.

Sunday Oliseh ataanza kibarua cha kukinoa kikosi cha Nigeria katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika dhidi ya Tanzania, mchezo utakaochezwa Septemba 5 jijini Dar es salaam.

Taarifa Za Seif Sharif Na Profesa Lipumba Kuvurugana Zapata Majibu
Maywether Kumalizia Ndondi Mwezi Septemba