Jeshi la Polisi Simiyu, limetoa elimu ya ulinzi na namna ya kufanya kazi kwa kuzingatia sheria za nchi kwa Viongozi wa vikundi vya ulinzi shirikishi zaidi ya 500 wa kanda ya ziwa, huku wakipewa onyo la kuacha kujichukulia sheria mkononi.
Elimu na onyo hilo vimetolewa na OCS wa kituo cha Polisi Maswa Mrakibu msaidizi wa Polisi, ASP Ramadhani Mkimbu katika eneo la Malampaka lililopo Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu, wakati wa mkutano wa pili wa viongozi wa sungusungu.
Amesema, “chombo chenye mamlaka ya kutoa hukumu ni Mahakama pekeyake, wewe Sungusungu mimi Polisi hatuna mamlaka kisheria ya kutoa hukumu kama baadhi yenu mnavyofanya”
Mkutano huo uliolenga kuwapa elimu ya pamoja Sungusungu wa kanda ya ziwa umehusisha maafisa wa Jeshi la Polisi kutoka Mkoa wa Mwanza, Shinyanga na Simiyu waliowasilisha mada mbalimbali kwa viongozi wa vikundi hivyo ili kuwapa uelewa wa pamoja kwenye masuala ya sheria na usalama wa wananchi.