Licha ya kuendelea kusuasua kwenye harakati za kusaka alama tatu za Ligi Kuu Tanzania Bara, Azam FC bado wana ndoto za kuwa mabingwa wa Ligi hiyo msimu huu 2020/21.

Kauli ya matumaini ya kuendelea kuwania taji la Ligi Kuu msimu huu, imetolewa na kiungo mkongwe wa klabu hiyo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ baada ya mchezo wa jana Jumatatu (Novemba 30) dhidi ya Biashara United Mara, uliomalizika kwa sare ya bao moja kwa moja.

Sure Boy amesema matokeo walioyapata jana dhidi ya Biashara United Mara ni sehemu ya mchezo wa soka, na bado wanaamini kikosi chao kina uwezo wa kufanya vyema katika michezo iliyosalia, na kutwaa ubingwa mwa msimu huu.

Amesema malengo yao hayawezi kuishia njiani kwa sababu ya kupoteza na kupata sare kwenye michezo kadhaa, hivyo watahakikisha wanarekebisha makosa yao, na kujipanga kwa ajili ya kuhakikisha wanashinda michezo ijayo.

“Kama timu ambayo ina malengo ya kutwaa ubingwa msimu huu ni wazi tulikuwa kwenye wakati mgumu sana kutokana na matokeo mabaya kwenye michezo yetu iliyopita.

“Lakini kwenye mchezo wa soka kuna wakati mnaweza kukutana na matokeo ambayo hamkuyatarajia na hatupaswi kukata tamaa, bali kurekebisha makosa yetu na kujipanga kwa ajili ya michezo yetu ijayo.”

“Ukiangalia nafasi tuliyopo kwenye msimamo na michezo tuliyocheza mpaka sasa utagundua kuwa bado tuna nafasi ya kupambania ubingwa msimu huu,” amesema Sure Boy.

Azam FC walianza Ligi msimu huu 2020/21 kwa kushinda michezo saba mfululizo, na kisha ilipunguzwa kasi baada ya kufungwa bao moja kwa sifuri dhidi ya Mtibwa Sugar, Uwanja wa Jamhuri.

Michezo mingine waliopoteza Azam FC ni dhidi ya KMC FC na Young Africans ambayo yote walipoteza kwa kufungwa bao moja kwa sifuri.

Azam FC wataendelea kusalia kanda ya ziwa wakisubiri kupambana dhidi ya Gwambina FC mwishoni mwa juma hili kwenye uwanja wa Gwambina, Wilayani Misungwi mkoani Mwanza.

Mdee: Hatuondoki CHADEMA
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Desemba 1, 2020