Jumla ya watu 267, 261 wamefikiwa na elimu ya chanjo ya Surua Wilayani Mlele Mkoani Katavi kwa njia ya magari ya matangazo na sinema huku watoto 43,384 wakipatiwa chanjo hiyo.
Takwimu hizo, zimetolewa na Afisa Programu Elimu ya Afya kwa Ummma, Idara ya Kinga, Wizara ya Afya Simon Nzilibili Mpimbwe Wilayani Mlele Katavi wakati wa kuhitimisha kampeni ya siku 14 ya Elimu na Uhamasishaji wa chanjo ya Surua.
Akizungumza kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Elimu ya Afya kwa Umma,Idara ya Kinga, Wizara ya Afya, Dkt. Haonga, Nzilibili amesema katika kipindi cha takriban wiki tatu, wawakilishi kutoka Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Timu za Afya za Halmashauri na Mkoa wamefanikiwa kufikia wananchi wengi na kuhamasika wazazi na walezi kuwapeleka watoto kupata chanjo.
“Katika kampeni hii ya kutoa elimu na kuhamasisha chanjo ya Surua kwa njia ya magari ,njia ya sinema na kampeni ya nyumba kwa nyumba tumeweza kufikia watu 267, 261 na hii imesaidia sana wazazi na walezi wengi kuwa na hamasa, ”amesema Nzilibili.
Kuhusu takwimu za chanjo ya Surua, Nzilibili amesema jumla ya watoto 43,384 wamepata chanjo ya Surua katika Halmashauri ya Mpimbwe ya Wilayani Mlele, Katavi.