Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, Sven Vandenbroeck amesema ushindi mnono wa mabao saba kwa sifuri walioupata juzi Jumamosi (Novemba 21), umewapa picha ya kufanya vizuri kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza wa hatua ya awali Ligi ya Mabingwa Afrika, dhidi ya Plateua United ya Nigeria.

Kikosi cha Simba SC kimeweka kambi mjini Arusha kikijiandaa na mchezo huo utakaopigwa mjini Jos, Nigeria mwishoni mwa juma hili, ikiwa ni mara ya kwanza kwa timu hizo kukutana.

Kocha Sven amesema licha ya matokeo dhidi ya Coastal Union kuwapa mwanga wa kwenda kupambana vyema ugenini, bado anaamini mchezo dhidi ya Plateau United hautakuwa mwepesi.

“Ushindi mbele ya Coastal Union ni furaha kwetu na unatupa picha ya kile ambacho tunakihitaji ndani ya Ligi ya Mabingwa Afrika licha ya kwamba sio kazi nyepesi.

“Kila mchezaji ameonekana kufurahi na inaleta matumaini kwamba tutakwenda kupambana ili kufanya vizuri, malengo yetu ni kuona kwamba tunapata ushindi,” amesema.

Kikosi cha Simba kinatarajiwa kuondoka nchini keshokutwa Jumatano, Novemba 25 kuelekea Nigeria kwa ajili ya kujiweka sawa kwa mchezo wa awali unaotarajiwa kuchezwa kati ya Novemba 27-29.

Kagere, Miquissone watinga kambini Arusha
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Novemba 23, 2020