Uongozi wa chama cha soka nchini Iraq umeonyesha nia ya kutaka kufanya kazi na aliyewahi kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya England Sven-Goran Eriksson, ili kufanikisha malengo ya nchi hiyo kucheza na kushinda mataji ya michuano mikubwa barani Asia na duniani.
Eriksson tayari ameshakutana na muwakilishi wa chama cha soka nchini Iraq katika mkutano maalum uliofanyika mjini Istanbul, Uturuki juma hili, na imeriporiwa mazungumzo baina ya pande hizo mbili yalikwenda vizuri.
Chanzo cha habari hii kimeeleza kuwa, huenda kocha huyo kutoka nchini Sweden akakutana rasmi na uongozi wa chama cha soka nchini Iraq siku ya jumatatu, kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya mwisho, kabla ya kusaini mkataba wa kuanza kazi.
Hata hivyo chanzo hicho cha habari kimeeleza kuwa, kocha huyo mwenye umri wa miaka 70, bado hajafanya maamuzi sahihi kama ataweza kukubali ofa itakayowasilishwa mbele yake mwanzoni mwa jma lijalo.
Iraq inatarajia kushiriki fainali za mataifa ya barani Asia mwaka ujao, na viongozi wa chama cha soka nchini humo wameweka dhamira ya kutwaa ubingwa wa michuano hiyo, kama walivyofanya miaka 12 iliyopita.
Nchi hiyo imepangwa kundi moja na Iran, Vietnam na Yemen, na michuano itaanza rasmi Falme Za Kiarabu Januari 5.
Eriksson, anakumbukwa na mashabiki wa soka duniani, baada ya kuifikisha England hatua ya robo fainali katika michuano ya kombe la dunia mwaka 2002, na hajawahi kufanya kai ya kuzinoa timu za taifa tangu mwaka 2010 alipoachana na Ivory Coast.