Kocha mkuu wa wawakilishi wa Tanzania Bara kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika Simba Sven Vandenbroeck, amesema kikosi chake bado kina kazi kubwa ya kufanikisha safari ya kutinga hatua mtoano ya michuano hiyo, licha ya kupata ushindi wa bao moja kwa sifuri dhidi ya Plateau United jana Jumapili (Novemba 29).
Bao lililofungwa na kiungo kutoka Zambia Clatous Chama lilitosha kuwapa kicheko Simba SC ugenini, kabla ya kurudi nyumbani Tanzania kwa mchezo wa mkondo wa pili Desemba 05, Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Kocha Sven amesema Plateau Unitd walionyesha soka la upinzani na walitumia nguvu wakati wote, lakini umahiri wa wachezaji wake ulifanikisha ushindi huo, ambao ulikua unasubiriwa na watanzania.
“Wapinzani wetu wana nguvu na walijaribu kiufundi kutafuta goli lakini walishindwa kutokana na uimara wa wachezaji wangu katika hilo ninawapongeza.
“Matokeo tuliyopta ni mazuri lakini bado hatujamaliza kazi kwa sababu wiki ijayo tuna dakika 90 zingine.” Amesema kocha Sven.
Katika mchezo wa mkondo wa pili Simba SC watahitaji ushindi ama sare ya aina yoyote ili wasonge mbele hatua ya mtoano.
Wakati Simba wakiwa nyumbani Desemba 05, wawakilishi wengine wa Tanzania Bara kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika Namungo FC, watakua ugenini Sudan Kusini wakicheza dhidi ya Al Rabita.
Mchezo wa mkondo wa kwanza uliopigwa Jumamosi (Novemba 28) Uwanja wa Azam Complex Chamazi, Namungo FC walichomoza na ushindi wa mabao matatu kwa sifuri.