Kocha wa zamani wa Simba SC Sven Vandenbroeck amesifia mashabiki wa klabu hiyo lakini akataja changamoto zilizoko kwenye viwanja vya mikoani.
Kocha Sven amekwenda mbali zaidi na kufunguka kinachoendelea katika kutakiwa na Simba SC na Klabu za Afrika Kisini.
“Niko tayari kufundisha Simba SC au Afrika kusini.” Kocha huyo Mbelgiji amesema kupitia mtandao wa Diski Times wa Afrika Kisini
“Naijua klabu na mazingira yake, wana mashabiki wengi wenye mapenzi na timu. Wana faida ya Ligi ya Mabingwa, lakini kwenye mechi za mikoani kuna changamoto. Ligi ya Afrika Kusini ni kubwa na rasilimali zao ni nzuri zaidi.” amesema Sven ambaye yupo kwenye orodha ya makocha watano Simba SC inaowataka.
Kocha huyo mwenye miaka 44, amesema matatizo mbalimbali ndiyo yaliyomsababisha kukaa kwenye klabu za Morocco na Algeria kwa muda mfupi.
“Pale Wydad nilisaini miezi minne kwa sharti la kubeba ubingwa wa Afrika tukapoteza kwa Ahly, CRB ni tofauti nilikataa kupangiwa timu na viongozi.” amesema Sven ambaye baadhi ya viongozi wa Simba SC wanaamini misimamo yake itawanyoosha baadhi ya mastaa wao.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba SC, Salum Abdallah ‘Try Again’ amesema ni kweli Simba SC inasaka kocha lakini watawatangazia mashabiki wao watakapompata kocha sahihi.
Akizungumzia suala la kocha baada ya kutajiwa jina la Sven amesema ni kocha mzuri aliacha rekodi nzuri ndani ya Simba SC na amefanya mambo makubwa Morocco
“Ni kocha mzuri lakini siwezi kusema ndiye anayeweza kuja kuinoa Simba SC ila mashabiki na wanasimba wanatakiwa kufahamu tutamleta kocha mzuri anayelifahanmu soka la Afrika na Ligi ya Mabingwa. “Lengo ni kuona anatuongoza kuanzia tulipo na kutufikisha sehemu kubwa ambayo tumekuwa tukiitamani muda mrefu hatua ya Nusu Fainali Ligi ya Mabingwa na mchakato wake unaenda vizuri anaweza kuja kabla ya mchezo wetu wa hatua ya makundi nyumbani au baada.” amesema Try Again