Kocha Mkuu wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Simba SC, Sven Vandenbroeck amesema anaamini kikosi chake kitafuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kwa kuitoa FC Platinum ya Zimbabwe katika mchezo wa mkondo wa pili utakaopigwa Desemba 06, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Sven ametamba kuwa na uhakika huo, huku akithibitisha kuwa na mbinu ambazo anaamini zitasaidia kufikia lengo la kuibuka na ushindi utakaolipa kisasi cha kupoteza mchezo wa mkondo wa kwanza uliochezwa mjini Harare, Desemba 23 ambapo Simba SC ilikubali kufungwa bao moja kwa sifuri.
Kocha huyo kutoka nchini Ubelgiji amesema nafasi bado ipo wazi kwa Simba SC, na bahati nzuri mchezo wa mkondo wa pili kikosi chake kitakua nyumbani, ambapo pamekua na bahati kubwa ya kupatikana kwa matokeo mazuri.
“Bado tuna nafasi kubwa ya kufuzu hatua ya makundi licha ya kupoteza mchezo wa kwanza, tunaamini tutapata matokeo mazuri katika mchezo wa marudiano tukiwa kwenye uwanja wa nyumbani.”
“Tunaendelea kufanya maandalizi ya nguvu kwa sababu hatukupoteza mchezo wa kwanza kutokana na ubora wa wapinzani, bali imetokea kutokana na makosa ambayo tulifanya,” amesema.
Sven amesema wanachokiangalia kwa sasa ni mchezo wa pili, wakiwa nyumbani, jambo ambalo anaamini watakuwa na nguvu kubwa ya kupambana na kuweza kupindua matokeo.
“Kikubwa kwa sasa ni kuangalia timu inataka nini kiufundi baada ya kuwaona wapinzani wetu, tunataka matokeo makubwa nyumbani,” alisema Sven.
Simba kwa sasa ipo katika presha kubwa ya kushinda mchezo huo ili kufuzu hatua ya makundi, lakini kuhakikisha haipotezi alama kwenye michezo yake ya Ligi Kuu, ili kuweza kupunguza wigo wa alama dhidi ya Young Africans wanaoongoza msimamo wa Ligi kwa kufikisha alama 43.
Endapo Simba SC itashinda michezo yake yote viporo ya Ligi Kuu, itafikisha pointi 41, alama mbili nyuma ya Young Africans, hivyo kuendelea kutoa upinzani katika mbio za kutetea ubingwa wake, wakati huu ikitaka kutwaa taji hilo kwa mara ya nne mfululizo.