Mabingwa wa Soka Barani Afrika Wydad AC wanakwenda katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Nusu Fainali, Ligi ya Mabigwa Barani humo dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini wakiwa na Kocha Mkuu Mpya baada ya kuachana na Kocha Juan Carlos Garrido.
Wydad AC iliyoiondoa Simba SC ya Tanzania katika hatua ya Robo Fainali mwishoni mwa juma lililopita, itaingia katika mchezo wa Nusu Fainali ikiongozwa na Kocha Mkuu kutoka Ubelgiji Sven Vandenbroeck.
Uongozi wa Klabu hiyo ya nchini Morocco umemtangaza Kocha huyo jana Ijumaa (Mei 05), akitokea Klabu ya Abha ya Saudi Arabia.
Vandenbroeck ambaye amewahi kufanya kazi na Simba SC, ni mzoefu wa Soka la Morocco kwani alikuwa Kocha Mkuu wa AS FAR msimu wa 2021–2022.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 43 atalazimika kushinda mchezo wa Nusu Fainali dhidi ya Mamelodi Sundowns Jumamosi (Mei 13) katika Uwanja wa Mohamed V mjini Casablanca-Morocco, kabla ya mchezo wa Mkondo wa Pili utakaopigwa Pretoria-Afrika Kusini katika Uwanja wa Loftus Versfeld.
Kwa upande wa Ligi Kuu ya Morocco Kocha Vandenbroeck ana kibarua cha kupambania Ubingwa, ambapo kikosi chake kwa sasa kipo nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi kwa tofauti ya alama moja dhidi ya AS FAR yenye alama 51.
Timu hizo zimecheza michezo 24, na bado michezo sita kabla ya Ligi Kuu ya Morocco msimu huu 2022/23 haijafikia tamati.