Kikosi cha mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba SC, kinaendelea na maandalizi ya mchezo wa mkondo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya FC Platnum, utakaopigwa mjini Harere nchini Zimbabwe, Desemba 23, 2020.

Simba SC imeweka kambi mjini Harare tangu Ijumaa, Desemba 18) kwa ajili ya  mchezo huo, ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini Tanzania na Zimbabwe ili kufahamu nani atatinga hatua ya makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kocha Mkuu, Sven Vandenbroeck amesema lengo kubwa kuelekea mchezo huo wa Desemba 23 ni kupata ushindi utakaokiweka kwenye mazingira mazuri kikosi chake kabla ya mchezo wa mkondo wa pili utakaochezwa mapema mwezi ujao jijini Dar es salaam, Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Kocha Sven amesema anafahamu FC Platnum ni timu kubwa na yenye ushindani mkubwa, lakini anawaandaa wachezaji wake kukabiliana na hali hiyo, ili kufikia lengo la kupata ushindi ugenini.

“Malengo yetu ni kuona kwamba tunashinda na kupata matokeo mazuri kwenye mchezo wa kwanza kisha ule wa marudio nao tutapambana kusaka ushindi.

“Wapinzani wetu ni timu kubwa na imara ila haitupi mashaka kwa kuwa nasi pia tupo imara.” Amesema kocha huyo kutoka nchini Ubelgiji.  

Simba SC ilitinga hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa kuifunga bao moja kwa sifuri Plateau United ya Nigeria, huku FC Platnum wakiitoa Costa do Sol ya Msumbiji kwa jumla ya mabao manne kwa moja.

Kata 27 hazina shule za sekondari- Rukwa
Katibu Mkuu: Mkitoa majoho hapa ni aibu